Tarehe 28 Aprili 2022, Mhe. Maimuna Tarishi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu Geneva alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Baraza la Haki za Binadamu, Balozi Federico Villegas (Mwakilishi wa Kudumu wa Argentina).

Pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi alimpongeza kwa mara nyingine tena kwa kushika madaraka ya Rais wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa; pia kwa kuendesha na kusimamia kwa umahiri mkubwa kikao cha 49 cha Baraza hilo.

Aidha, Mhe. Balozi alimuhakikishia kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Uwakilishi Geneva itaendelea kushirikiana na Baraza la Haki za Binadamu na kwamba nchi ipo makini na imedhamiria kwa dhati kuendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia misingi ya Haki za Binadamu kwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Balozi Villegas alipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushiriki wake kwenye tathmini ya hali ya haki za binadamu na hususan kwa kuidhinishwa kwa Taarifa ya hali ya haki za binadamu na kwa kukubali kutekeleza mapendekezo mengi yaliyotolewa na wadau.

Aidha, ameelezea kuwa tayari kushirikisha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa majukumu na kazi mbalimbali za Baraza hilo.